Alhamisi, 27 Juni 2013

SAIKOLOGIA NA MAISHA. JINSI YA KUPATANA NA MTU

 
KWA kuwa migogoro ni moja kati ya mambo yanayotokea katika safari ya maisha si vibaya tukajifunza namna ya kuikabili. Kwa bahati mbaya tafiti zinaonyesha kuwa kiwango cha migogoro ni kikubwa miongoni mwa jamii ukilinganisha na watu wenye ufahamu wa kuitatua.
Watu wamekuwa wakifanyiana ukatili, nchi zikipigana vita kwa sababu ya migogoro mbalimbali ambayo ingepata wajuzi wa kuitatua isingeleta madhara makubwa. (L. Ron Hubbard Mtafiti wa Sayansi ya Jamii kutoka Marekani anathibitisha hili pia).
Zifuatazo ni mbinu za kufikia makubaliano na mtu uliyekosana naye.
KWANZA : Mgogoro unapotokea baina ya mtu na mtu au taifa kwa taifa kitu cha kwanza kabisa kufanyika ni kwa wahusika kutambua kuwa wameingia katika mgogoro na hivyo kutazama kwa kina madhara ya mgogoro na kuamua kutuliza jazba zao kwa lengo la kutazama namna ya kumaliza matatizo kwa njia ya amani.
Katika hatua hii hawatakiwi kutafuta nani mwenye makosa katika mgogoro huo bali ni wakati wa kuamua kukaa katika meza ya mazungumzo huku suala la nani mwenye makosa likishughulikiwa baadaye.
PILI : Mahali penye mgogoro kila mtu hupenda kusikilizwa, akiamini kuwa ana sababu za msingi zilizomfanya akasirike au akorofishane na mwenzake. Hivyo kwa mtu mwenye elimu na nia ya kutatua mgogoro atakuwa tayari kutoa nafasi kwa upande wa pili utoe dukuduku hata kama litakuwa limesheheni matusi na uongo. Usimkatize mwenzako anapotoa maelezo yake, nyamaza umsikilize mpaka mwisho akimaliza na wewe eleza yako.
TATU : Usikimbilie kujihukumu hasa pale wasuluhishi wanapojaribu kuchambua mambo kwa kuonesha dalili za kukuzonga na pengine kukuhukumu. “Oke, kama mimi nina makosa basi niacheni kaeni ninyi wasafi” Usiseme hivyo, vumilia lawama na pointi yako ya msingi iwe ni kwenye busara ya kulimaza tatizo.
NNE : Unapokuwa katika safari ya kutaka suluhu, pendelea sana kuunga mkono yale yanayozungumzwa kwenye kikao au anayozungumza mwenzako. “Ni kweli kabisa, hapo umesema sawa, nakubaliana na wewe” Kauli za kukubali kama hizi zina nguvu kubwa ya kuwafanya wajumbe au mgomvi mwenzako anyonywe hasira na kukuona ni mtu mwelewa unayestahili suluhu.
TANO: Kama utaona mgomvi wako bado amejaa hasira kiasi cha kutotaka kukusikiliza, sitisha mapatano na umruhusu aondoke au wewe uachane naye kwa muda. “Naona bado una hasira nyingi, tulia hasira zikipungua tutazungumza.”
Unapompa mwenzako muda zaidi wa kutafakari kiwango cha hasira hushuka na pengine kufikiria kwa kina madhara ya kugombana. Usilazimishe suluhu  wakati wa muwako wa hasira, ukifanya hivyo utakuza tatizo.
SITA: Mtakapofikia katika hatua za maelewano na ukabaini kuwa wewe ulikuwa na makosa katika mgogoro huo, uungwana unakutaka uwe mwepesi kukiri kosa na kutaka kumaliza tatizo. “Niliteleza naomba unisamehe.” Lakini hata kama umeona mwenzako ana makosa ila hataki kukubaliana na wewe, kuwa tayari kubeba lawama kwa lengo la kumaliza tatizo.
SABA: Jambo kubwa la mwisho linaloweza kusaidia kutatua migogoro ni kutumia nguvu ya ufahamu wako wa mambo. Kwa mfano; kama unaishi na mkeo  ama ndugu kwenye nyumba moja unatakiwa kumfahamu tabia zake na kuzichukulia hadhari, vivyo hivyo bosi wako, wafanyakazi wenzako, wanafunzi wenzio, waalimu wako, lazima uwafahamu tabia zao. Hii itakusaidia kutoingia katika mgogoro nao.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni